Tarehe 14 Februari 2025 Halmashauri ya Mji Njombe, kupitia Mkurugenzi wake Bi. Kuruthum Sadick, imetoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi 100 kutoka kwenye mazingira magumu. Mpango huu unalenga kuwawezesha watoto hao kuendelea na masomo yao bila vikwazo na kufanikisha ndoto zao za kielimu.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa rasmi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe, Mhe. Erasto Mpete, ambapo kila mwanafunzi amepokea begi la shule lililojaa vifaa muhimu ikiwemo madaftari, shati, kalamu, rula, na seti ya hisabati.
Wanafunzi waliopokea msaada huo walichaguliwa baada ya kufanyika upembuzi yakinifu kupitia idara za elimu halmashauri ya mji Njombe kufuatia matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2024. Wanafunzi hao wamefaulu na wamejiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025, lakini wanatoka katika familia zenye hali ngumu kiuchumi.
Mhe. Mpete alipongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa kuwa halmashauri itaendelea kusaidia wanafunzi kutoka katika mazingira magumu ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa elimu kwa sababu ya ukosefu wa mahitaji ya msingi.
Wanafunzi na wazazi wao walipokea msaada huo kwa furaha na kutoa shukrani kwa halmashauri kwa kuwasaidia katika safari yao ya kielimu. Mpango huu ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha elimu inapatikana kwa usawa kwa watoto wote katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe